![]() |
| MH.BERNARD MEMBE |
SERIKALI imesema eneo linalogombewa na Malawi katika Ziwa Nyasa ni mali ya Tanzania na sasa imeziamuru kampuni za nchi hiyo zinazofanya utafiti wa mafuta kuondoka eneo hilo kuanzia jana.
Onyo hilo dhidi ya Malawi lilitolewa jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye pia amesisitiza kuwa Tanzania itakuwa tayari dhidi ya tishio lolote la dhahiri au la kificho la kiusalama.
Hii ni mara ya pili Serikali kuionya Malawi katika mgogoro huo. Wiki iliyopita aliyekuwa Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni Samuel Sitta alisema: “Tuko tayari kwa lolote dhidi ya Malawi.”
Sitta alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu Swali la Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu mgogoro huo.
Jana, akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka 2012/13, bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisisitiza kwamba eneo linalobishaniwa katika ziwa hilo lipo Tanzania.
Alisema pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kuzipiga marufuku ndege za utafiti za kampuni hizo, bado zilikaidi na ndege tano zilitua katika eneo la Ziwa Nyasa.
“Serikali ya Tanzania inapenda kuzionya na kuzitaka kampuni zote zinazoendelea na shughuli za utafiti katika eneo hilo zisitishe mara moja kuanzia leo (jana),” alisema Membe.Alisema Serikali ya Tanzania iko tayari kulinda mipaka yake kwa gharama yoyote na haitaruhusu utafiti huo wa uchimbaji wa gesi na mafuta uendelee.http://mwananchi.co.tz

0 comments:
Post a Comment