10:1-22:16 MITHALIZA SULEMANI
Mithali
katika sehemu hii kwa jumla zimeandikwa kwa utunzi rahisi wa mistari miwili
miwili, na karibu kila mithali inafanana na mstari fulani katika Biblia yetu.
Ingawa mhariri aliyekusanya mithali hizo alijitahidi kujumlisha mithali zile
zinazohusika na somo moja au maana maalumu, inafaa kila mithali ifikiriwe kwa
ujumbe wake.
Ni wazi
kwamba hapa hatuna nafasi ya kueleza kila mithali peke yake. Msomaji anapata
faida zaidi akisoma kitabu cha Mithali pole pole na kwa uangalifu (kwa mfano
fungu moja tu kwa wakati mmoja, ili aweke nafasi ya kutosha kati ya mafungu
mbalimbali), akitulia na kuzingatia kila mithali na jinsi inavyohusika katika
maisha ya kila siku. Mithali hizo ni mifano mizuri jinsi hekima na ujinga
vilivyoelezwa katika mafungu ya 1-9, na vinavyoweza kuingizwa katika mazoea ya
kila siku.
Hekima katika maisha ya kila siku (10:1-32)
Mkusanyo
unafunguliwa kwa maelezo ya baadhi ya mawazo makuu ya sehemu zilizopita, yaani
hekima na ujinga, haki na uovu, uvivu na bidii; kwa kutilia mkazo juu ya
matokeo ambayo mambo hayo yanaleta kwa mtu binafsi na kwa watu wanaoishi karibu
naye (10:1-5). Matendo ya mtu yanaonyesha tabia yake, ikiwa ni njema au mbaya,
na sifa yake itaendelea hata baada ya kufa kwake (6-7). Mtu hujenga hekima kwa
njia ya kujifunza, wala si kwa njia ya kujisifu. Anapata usalama kutokana na
maisha ya unyofu, wala si kwa njia ya shughuli za hila (8-9).
Kuna watu
ambao kwa njia ya matendo ya hila na maneno ya ujanja wanachokoza matata. Kuna
wengine ambao kwa kusema wazi na kwa upendo huleta amani (10-12). Mwenye hekima
hutunza ujuzi wake ili autumie wakati ufaao; lakini mpumbavu husema wakati
usiofaa, na hivyo mara nyingi hujipatia shida (13-14).
Kwa muda
fulani fedha zinaweza kuongeza usalama wa mtu, lakini lazima zipatikane kwa
njia ya halali na zitumiwe kwa akili, kama
inatakiwa ziongeze thamani ya maisha (15-17). Mtu akiwa na chuki moyoni mwake,
maneno yake huwa na unafiki au yanachokoza. Afadhali maneno yake yawe kweli,
yaliyochaguliwa
vizuri ili yawasaidie wasikilizaji (18-21).
Wapumbavu
na wajeuri hujenga maisha yao juu ya vitu
viharibikavyo na vya muda mfupi, kwa hiyo wanaogopa sana misiba ya ghafla inayoweza kuwaangamiza.
Lakini kwa kweli mambo hayo yatawapata. Wenye haki wanajenga maisha yao juu ya mambo
yanayodumu. Kwa hiyo wanaendelea kuwa na usalama na utulivu, ingawa wanaweza
kukabiliwa na matatizo (22-25). Mvivu ni chukizo kwa mwajiri wake (26).
Mungu
anaahidi maisha marefu, furaha na ulinzi wake kwa watu wenye haki.
Anawahakikishia waovu kwamba, akichukua hatua dhidi yao ,
maisha yao
yatakwisha katika hali ya kukatisha tamaa (27-30). Usemi wa wenye haki una
hekima na wema, lakini ule wa waovu unadanganya na kuumiza (31-32).
Mafanikio, unyofu na utu wema (11:1-31)
Ni ujinga
mtu akijaribu kutajirika kwa mbinu zisizo na haki, kwa sababu ukosefu wa
uaminifu huleta hukumu wala mali
haiwezi kumwokoa (11:1-4). Mtu asiyekuwa na hatia ana uhakika wa kupata ushindi
wa mwisho, ila mwenye ujeuri hujiangusha mwenyewe (5-8). Watu wema wakiwa na
sauti katika utawala wa mji, wenyeji wake huishi katika usalama na furaha,
lakini kila mji una watu waovu wachokozao matata baina ya majirani na kuanzisha
wasiwasi katika jumuia (9-11). Kwa sababu ya matatizo yanayoletwa na watu hao
kwa usemi wao mbaya, viongozi wanapaswa kuweka sheria safi na yenye hekima (12-14).
Onyo
lingine linatolewa kuhusu utoaji wa dhamana ya haraka (15; taz. maelezo ya
6:1-5). Ujeuri unaweza kuleta mafanikio, lakini utajiri huo hauaminiki, kwa
sababu una muda mfupi tu. Kinyume chake, utu mwema huleta heshima ya kweli na
thawabu inayodumu (16-20). Mungu anatawala maisha ya watu wote, naye
anahakikisha kwamba maisha ya wenye haki tu ni maisha yenye maana (19-20). Kwa
watu wengine tofauti zinaonekana kati ya maisha yao ya ndani na hali zinazoonekana nje,
lakini mwisho haki itashinda (21-23).
Matokeo ya
fadhili hayatakuwa umaskini, kwa sababu Mungu atatoa thawabu yake. Lakini watu
wanawalaani wale ambao wakati wa njaa kali wanaficha chakula kwa makusudi ya
kupandisha bei yake (24-26). Haidhuru mtu anatazamia kitu gani, ikiwa ni wema
au ubaya, atakipata, lakini akitafuta usalama
kwa njia ya
kukusanya mali nyingi atakatishwa tamaa (27-29). Mwenye haki kwa
maisha yake mema huleta baraka kwa watu wengine. Iwapo hata yeye mara nyingine
anapata taabu kutokana na hukumu ya haki ya Mungu, zaidi sana mtu mwovu atapata shida kali mno
(30-31).
Maneno ya kweli na kazi yenye haki (12:1-28)
Kuna
mithali nyingine juu ya tabia ya kuvumilia lawama au kutaja makosa ya watu
(12:1-2; taz. maelezo ya 9:7-9), juu ya maisha imara ya mwenye haki (3) na
thamani ya mke mwema (4). Mtu mwenye haki, licha ya kuwa na kanuni safi , pia ana ujasiri wa
kusema wazi bila ya kuogopa kujihatarisha, ili aweze kuwaokoa watu wengine
(5-7).
Watu
wakiishi katika unyenyekevu kadiri ya uwezo wao wa kujimudu, labda watakosa
kupata sifa ya kuwa na hali ya juu, lakini wanaishi bila deni. Wana hekima
kuliko wale wanaotumia pesa ovyo, ili kujivuna mbele ya watu wengine, lakini
mwisho wana njaa na umaskini (8-9). Hali kadhalika ni afadhali watu wakihakikisha
usalama wao kwa njia ya kufanya kazi ngumu, kuliko kupoteza wakati na fedha kwa
mambo yasiyofaa. Kazi ya uaminifu na usemi wa kweli huheshimiwa na watu na
kuwaridhisha wenye tabia hiyo (10-14).
Watu wenye
busara husikiliza ushauri na kudharau maneno ya kuwaaibisha (15-16). Daima
husema yaliyo kweli, lakini maneno yao
husaidia na kuponya kuliko kuumiza (17-19). Wakifanya hivyo wanampendeza Mungu
na kujaza furaha moyoni mwao (20-22). Wenye busara hukaa kimya kuliko kuonyesha
ujuzi wao bure, lakini siku zote watakuwa na neno la kufaa kwa kumtia mtu moyo
na kumwongoza anayehitaji msaada kama huo
(23-26). Kinyume chake wavivu, kamwe hawapati wanachotaka, nao wanaweza
kutawaliwa na wengine (23-28).
Kuridhika katika ugumu wa maisha (13:1-25)
Ushauri unaotolewa
na wazazi ni jambo bora katika maisha. Watu wakataao ushauri huo daima, hujenga
tabia ya kudharau mashauri yote isipokuwa yao
wenyewe tu (13:1). Maneno mema huleta thawabu, lakini matokeo ya maneno ya hila
ni ujeuri. Nidhamu katika usemi ni muhimu, kwa sababu maneno makali huleta
uharibifu (2-3). Nidhamu pia inatakiwa katika kazi na maisha yote, la sivyo
maisha ya mtu huishia katika uharibifu. Usalama hupatikana katika uaminifu
(4-6).
Mara
nyingine maskini anaweza kujionyesha kana kwamba ni tajiri (kwa sababu kuna
faida fulani katika mali ),
lakini matajiri, kwa sababu ya ubahili, wanaweza kujionyesha kana kwamba ni
maskini (7-8). Watu wakipata utajiri haraka, mara nyingi wanatumia mali yao
bila uangalifu. Mali
iliyopatikana pole pole kutokana na kazi ngumu inadumu zaidi (9-11).
Watu
wakiona matarajio yao
yakitimizwa wanafurahi; wakikubali mafundisho ya wenye hekima wataburudishwa
(12-14). Wakiwa na akili safi
ya kawaida wataheshimiwa na watu na wenyewe watafurahi. Watapata matarajio yao . Lakini wapumbavu
hawana akili ya kutosha kwa kuficha ujinga wao wala kwa kuepukana na njia
zinazowaletea uharibifu (15-19). Kufanikiwa katika maisha kunategemea sana watu ambao mtu
anashirikiana nao (20-21).
Inaonekana
kama kuna haki fulani, iwapo matajiri waovu wanapotelewa na mali yao
waliyojipatia kwa njia ya kuwanyanyasa maskini. Ingawa kwa kawaida dhuluma
inapinduliwa siku moja, wazazi hawana budi kuamua mashauri yao kwa haki iwezekanavyo wakati huo
wanapowafundisha watoto wao na kuwaandaa kwa siku za usoni (22-25).
Hisia, tabia na makusudi (14:1-35)
Hekima
hujenga, lakini ujinga hubomoa. Tabia ya mtu ya kumheshimu Mungu hudhihirishwa
kwa matendo yake (14:1-2). Kati ya mambo yanayoamua kama
mtu atakuwa na maendeleo mazuri au atafilisika ni hekima katika usemi wake na
tabia yake kuhusu kazi ngumu (3-5). Mtu anayefikiri kwamba anajua mambo yote,
kamwe hawezi kuwa na hekima ya kweli, na hivyo hatakuwa na utambuzi mzuri
kuhusu maadili mema ya maisha (6-8).
Watu wema
wanaweza kufanikiwa na waovu wanaweza kupata hasara, lakini moyoni mwa mtu,
hata akiwa mwema sana ,
huzuni fulani inaweza kufichika ambayo hakuna mtu awezaye kuishiriki (9-14).
Mtu aaminiye kila neno, atupaye mbali tahadhari yo yote, au afanyaye mambo yake
kwa tabia ya harara, anazidisha shida ya ujinga wake tu (15-18). Mtu mwovu
anaweza kuwaheshimu watu wema moyoni mwake, lakini anawadharau kabisa maskini,
kwa sababu anajua kwamba hawezi kupata kitukwao (19-21).
Mithali
tano zinazofuata zinahamasisha makusudi safi ,
bidii ya kazi, hekima, usemi wenye ukweli na heshima kwa Mungu (22-27). Hakuna
mtu awezaye kuishi bila ya kuwategemea wengine; hata mfalme hawezi kuishi bila
raia zake (28). Tabia mbaya inaharibu afya ya mtu pamoja na utu wake wa ndani,
lakini unyanyasaji wa maskini huharibu uhusiano wake na Mungu (29-31). Hekima
na haki huleta faida katika kila hali zinapotumiwa, ikiwa ni katika maisha ya
binafsi au katika mambo ya siasa ya taifa lote (32-35).
Kuwafurahisha watu wengine (15:1-33)
Maneno
yanaweza kuwafurahisha watu au kuwachokoza; kuwasaidia au kuwarudisha nyuma.
Kwa hiyo ni muhimu sana
mtu afikiri vizuri maneno anayotumia (15:1-5). Licha ya kuwa na busara katika
usemi wake, lazima mtu awe na uaminifu katika njia za kujipatia riziki yake
(6-7). Kwa kweli, hana budi kuwa mnyofu katika sehemu zote za maisha yake. Hapo
tu Mungu ambaye mbele yake hakuna linalofichika, atapokea sadaka zake na maombi
yake (8-11). Jambo lingine linalohusu usemi wa mtu ni kwamba, yule ambaye
hupenda sana
kuwaonya wengine, mara nyingi hukasirika akionywa mwenyewe (12).
Furaha ya
moyoni humwezesha mwamini achangamke hata akiwa katika matatizo. Kwa kuwa
anamcha Mungu kwa kweli na kuwapenda watu wengine, anaridhika hata asipokuwa na
mali
(13-17). Mfululizo wa maonyo unaonyesha kwamba matendo mabaya huleta taabu
kubwa: tabia ya hasira huleta mabishano (18), uvivu humlazimisha mtu afanye
kazi ngumu zaidi baadaye (19), ujinga huleta ugomvi nyumbani (20) na matokeo ya
upumbavu ni kuharibika kwa mipango (21-22).
Watu
wanaowafurahisha wengine wanahakikishiwa kupata wema wa Mungu (23-24), lakini
Mungu huwapinga wale wanaofanya fitina na wanaotumia daraja lao la juu ili
kuwanyanyasa maskini na wasioweza kujitetea (25-29). Sura ya mtu anayechangamka
ni kama habari njema inayowaburudisha watu
(30). Kitabu kinaendelea kueleza kwamba, ili kupata hekima watu hawana budi
kujifunza, wamheshimu Mungu na wawe na roho yenye unyenyekevu (31-33).
Kupanga mikakati na uamuzi (16:1-33)
Mtu anaweza
kuwa na maarifa na kupanga mikakati, lakini ni Mungu tu aamuaye matokeo yake,
kwa sababu
Yeye anajua hisia za mtu na kutawala matukio kadiri ya makusudi yake mwenyewe.
Kwa hiyo ni muhimu kabisa kumwingiza Mungu katika mipango yote (16:1-4). Mungu
anawaadhibu wenye kiburi na kuwahurumia waaminifu (5-6). Anawalinda wasipate
shida na kuwaongoza katika njia za haki (7-9).
Iwapo
hekima ya mfalme hutoka kwa Mungu, maamuzi yake huwa ya haki. Hataonyesha
upendeleo, bali ataadhibu uovu, atasifu wema na kuangalia kwamba biashara zote
zinaendeshwa kwa haki na amani (10-15). Tajiri wa kweli si mtu aliye na fedha
nyingi, bali ni yeye aliye na hekima, unyofu, unyenyekevu, utiifu na uaminifu
(16-20).
Usemi mwema
hauna unafiki kama umetoka katika moyo safi .
Unampa faida msemaji wake kwa sababu unayapa maneno yake ushawishi mwema na
kuwapa wasikilizaji faida ya kujenga mawazo yao (21-24). Mtu anaweza kujidanganya
mwenyewe, lakini hawezi kuepukana na ukweli kwamba asipofanya kazi, atalala na
njaa (25-26). Kinyume cha usemi mwema uliotajwa sasa hivi, kunong'ona na kutoa
mashauri ya ujanja huleta matata tu (27-30). Kuishi maisha ya unyofu
huthibitisha heshima katika uzee. Kujitawala huthibitisha nguvu, na kuweka
mambo yote mbele ya Mungu humpa mtu uamuzi uliosawa (31-33).
Marafiki na wajinga (17:1-28)
Maisha ya
amani katika nyumba ni baraka kubwa, haidhuru watu wake wakiwa na hali ya
chini; lakini mwana anaweza kukosa urithi wa familia yake kwa sababu ya ujinga
wake (17:1-2). Matendo ya Mungu na watu wake siku zote yana makusudi mema, ili
kuwafanya kuwa wema kuliko walivyokuwa awali (3). Kusikiliza maneno mabaya ni
vibaya sawa sawa na kuyasema mwenyewe; kufurahia matatizo ya watu wengine ni
vibaya sawa sawa na kuyasababisha mwenyewe (4-5).
Mithali
nyingine zinahusika na uhusiano mwema ambao wazee na vijana wanapaswa kuwa nao
(6), umuhimu wa usemi unaofaa (7), mafanikio yanayopatikana rahisi kwa kutoa
rushwa isivyo halali (8), na tabia mbalimbali za wapatanishi na waletao ugomvi
(9).
Wapumbavu
ni watu wa hatari, kwa sababu ni wakaidi na waasi wala mtu hawezi kujadiliana
nao (10-13). Kwao kutoelewana kidogo kunaweza kuchokoza ugomvi mkubwa.
Wanafikiri kwamba wakimlipa mwalimu ada yake, wamekwisha pata hekima, lakini
hawana nia ya kujifunza neno (14-16).
Mtu akiwa
na shida anaweza kumtegemea rafiki wa kweli na kupata msaada, lakini asitazamie
msaada huo upite kiasi kwamba rafiki huyo afilisike (17-18). Mtu ambaye kwa
njia ya matendo ya kinyume hujiendeleza ili aweze kujivunia hali ya daraja la
juu anachokoza uangamizi (19-20). Upumbavu huleta huzuni, na huzuni ya daima
huharibu afya ya mtu. Kinyume chake, uchangamfu humsaidia mtu kuwa na afya
njema (21-22). Watu wasio na hatia huteswa na
maafisa wanaodai rushwa,
na wazazi wa mpumbavu hupata huzuni kwa sababu ya
upumbavu wa mwana wao. Mpumbavu hutanga tanga bila makusudi, lakini mwenye
bidii hufikiri matendo yake yote kwa akili (23-26). Alama ya hekima ni kufikiri
kabla ya kusema (27-28).
Kutajwa kwa rushwa na ushuhuda wa uongo mara nyingi
kunadokeza jinsi mahakama yalivyochafuka kwa mambo hayo wakati wa kuandikwa
mithali hizo; taz.l4:5,25; 17:8,15,23,26; 18:5; 19:5,9,28).
Nguvu ya kweli (18:1-24)
Inawezekana
kwamba mtu anaamini sana
mashauri yake mwenyewe hata akawaacha marafiki zake wa zamani, akishindwa
kujadiliana na watu, naye huwa kipofu kwa mawazo ya watu wengine. Watu
wanaodharau wengine, wenyewe wataaibishwa (18:1-3). Maneno ya mwenye hekima
huburudisha, lakini maneno ya mpumbavu au ya mpiga domo huharibu (4-8). Mtu
aachaye kazi bila ya kuimaliza hufanana na mtu anayeharibu kilichotengenezwa
(9). Mtu anayemtegemea Mungu anajua kwamba yu salama; ila mtu ategemeaye mali yake
anafikiri kwamba yu salama, lakini siku moja atatambua kwamba kiburi huleta
uharibifu (10-12).
Nguvu ya
akili na uthabiti wa roho ni bora katika vita vya maisha kuliko nguvu za
kimwili. Mwenye hekima husikiliza ushauri kutoka kila upande uwezekanao kabla
ya kutoa uamuzi wake. Lakini mara nyingine watu wanaweza kujaribu kupata kibali
kwa njia ya kutoa zawadi, na mara nyingine labda wanapaswa kupiga kura ili
kuamua jambo gumu (13-18). Mtu anaweza kuwa rafiki sana au adui mkali wa mtu kutokana na jinsi
anavyotendewa. Matunda ya maneno ya mtu humrudia mwenyewe kwa wema au kwa ubaya
(19-21). Urafiki wa kweli hauvunjiki upesi wala hautofautishi baina ya tajiri
na maskini. Lakini mke mwema ni rafiki bora kuliko wote (22-24).
Mafundisho yanayokubaliwa na yanayodharauliwa
(19:1-29)
Ni muhimu
zaidi kuwa mnyofu katika maadili kuliko kuwa tajiri, kutimiza mambo kwa
uangalifu kuliko kuyamaliza kwa haraka ya kuhangaika. Watu wasimlaumu Mungu kwa
shida waliyojipatia wenyewe kwa njia ya makosa yao (19:1-3).
Mara nyingi
sababu ya tajiri kuwa na marafiki wengi ni kwamba, 'marafiki' hao hutegemea
kupata faida yao binafsi kutokana na mali au uwezo
wa tajiri huyo (4-6). Upande mwingine, maskini hupoteza marafiki zake, ingawa
kwa namna fulani ni tajiri akiendelea kuwa na hekima yake (7-8). Afadhali kila
mtu aishi kadiri ya hali na uwezo wake katika jumuia, ingawa kutojali ukweli
siku zote ni vibaya (9-10). Akiwa na busara ya mtu aliyekomaa, hatakubali
kuchukuliwa na hasira upesi, naye atajua jinsi ya kujitawala (11-12).
Upumbavu,
ugomvi, uvivu na ukosefu wa nidhamu ya wazazi huharibu furaha ya familia.
Matendo yenye hekima, huruma na uthabiti wa wazazi hujenga nyumba hiyo (13-18).
Mtu mwenye tabia ya harara anaonekana kama
hawezi kujifunza kamwe, na matokeo yake, daima hujiletea taabu (19-20).
Mungu
huongoza mambo ya maisha ya watu, naye anatazamia kwao uaminifu na utii.
Anawabariki wale wanaomtii, lakini si wale walio wavivu (21-24). Mapigo ya
fimbo mara nyingine ni njia ya pekee ya kumrekebisha mpumbavu, lakini mtu mwenye
busara husikiliza akionywa na kujifunza kutokana na makosa yake (25-29).
Uaminifu (20:1-30)
Mtu mwenye
hekima hatakuwa mlevi, hatawachokoza wenye mamlaka bila sababu maalumu,
atakwepa ugomvi, naye atafanya kazi ili ajipatie riziki yake (20:1-4). Pia
atakuwa na uwezo wa kutambua mawazo na makusudi ya ndani ya mtu anayeshughulika
naye (5). Watu wengi hujisifu kuhusu uaminifu wao, lakini wachache tu ni
waaminifu kweli. Kuishi katika uaminifu ni njia bora kwa mtu kuwahakikishia
watoto wake maisha bora kwa wakati wa usoni (6-7). Mfalme hujifunza kutokana na
uzoefu wake kuamua kati ya wema na ubaya katika mambo yanayoletwa mbele yake
ili atoe uamuzi, lakini pia anajua kwamba moyo wake, sawasawa na mioyo ya
wanadamu wote, hauwezi kuwa bila dhambi (8-9).
Mungu
huchukia udanganyifu. Iwapo hata mwanadamu kwa njia fulani anaweza kutambua
hali ya moyo wa mtu mwingine kutokana na matendo yake, sembuse Mungu
aliyewaumba wanadamu (10-12). Mfanyakazi mwaminifu huridhika akijua kwamba
riziki yake anapata kwa njia ya haki; lakini mnunuzi mwenye hila apataye kitu
bora kwa bei rahisi (kwa sababu alikilaumu mbele ya mwenye mali ), kujisifu
kwake hakuna muda mrefu. Watu wengine hawaaminiki, kwa hiyo mtu aangalie sana wakati wa kukopesha pesa, naye ahakikishe kufanya
usalama fulani wa dhamana au rehani ili arudishiwe mali yake (13-17). Mtu mwenye
hekima husikiliza ushauri, hukwepa porojo na kuwaheshimu wazazi wake jinsi
inavyompasa (18-20).
Kutotulia
humsababisha mtu kukosa, ikiwa ni katika kungojea urithi wa agano fulani, au
katika kutaka kumwona mkosaji aadhibiwe, au katika kuahidi nadhiri kubwa kwa
haraka. Utulivu humwezesha mtu kumngojea Mungu naye ataongoza mambo yote
(21-25). Adhabu za mfalme zinaweza kuwa kali, lakini lazima ziwe na haki (26).
Inafaa dhamiri ya mtu imwonyeshe makosa yake ili aweze kujirekebisha, lakini
mara nyingine dhamiri yake haifanyi kazi vizuri, na hapo adhabu ya kuumiza
zaidi inatakiwa ili kusawazisha makosa yake (26-30).
Mungu hushughulika na wanadamu (21:1-31)
Kama vile
Mungu anavyoongoza mkondo wa mito ,
ndivyo anavyoongoza uamuzi wa watawala wa mataifa kadiri ya makusudi yake
(21:1). Mungu anajua makusudi ya wanadamu naye hatakubali sadaka zao, iwapo
mawazo na matendo yao
ni kinyume (2-4). Mafanikio yanayotokana na bidii ni thawabu njema; mafanikio
yanayotokana na ubahili, uongo na ujeuri ni mtego uletao mauti (5-8). Watu
wengine hufanya maisha kuwa magumu sana
kwa wale waishio pamoja nao katika nyumba moja, na wengine wanatazamia kufanya
uovu kwa makusudi po pote wanapoweza. Watajiharibu wenyewe, lakini wenye haki
watafurahia baraka (9-12).
Mtu anaweza
kuishi kwa ajili ya faida yake binafsi tu, akiwadharau wenye dhiki na kuwapa
rushwa wenye uwezo ili apate kitu cho chote anachokitaka ili aishi katika
starehe. Ni haki kama siku moja atapata shida
kutokana na ubinafsi wake na kutokuwa mwaminifu (13-17). Hivyo akiteswakwa
ajili ya uovu aliomkusudia mtu asiye na hatia, mtu mwovu huwa fidia au badala ya mwenye haki
(18). Mwenye hekima huweka akiba kwa ajili ya siku zijazo, wakati huo huo
akitambua kwamba, njia ya pekee ya kupata mali idumuyo ni kutenda haki na
fadhili (19-21).
Hekima ina
faida zaidi kuliko nguvu ya kijeshi, na kutawala ulimi ni silaha bora dhidi ya
matatizo (22-23). Matendo ya kidini yakitimizwa kwa makusudi ya kinyume ni
chukizo kwa Mungu, pamoja na kiburi, uvivu na tamaa ya ubinafsi (24-27). Mtu
anapaswa kutoa ushuhuda maalumu kuhusu mambo anayoyajua, wala si kuonyesha sura
yenye ujasiri tu ili atafute heshima ya watu (28-29). Ni bure kabisa kushindana
na Mungu, pia ni bure kushindana au kupiga vita bila Yeye (30-31).
Watoto na watu wazima (22:1-16)
Watu
wanatofautiana katika hali na sifa zao, lakini wanapaswa kuheshimiana wakijua
kwamba wote ni viumbe vya Mungu bila tofauti ya thamani yao (22:1-2). Mwenye hekima hutimiza matendo
yake kwa uangalifu na unyenyekevu. Hulea watoto wake ili awaandae kwa maisha
yanayowakabili (3-6). Mtu akopaye atakuwa chini ya mamlaka ya mkopeshaji, na
hali hiyo inaweza kusababisha kuonewa kwa maskini na matajiri. Lakini dhuluma
ya namna hiyo itaadhibiwa, ambapo fadhili italeta thawabu (7-9).
Watu
wanapojaribu kufanya kazi pamoja kama kikundi,
lazima waelewane na kupatana. Ni afadhali kuondokana na mtu aletaye ugomvi
daima kuliko kuendelea naye. Upande mwingine, mtu asemaye kweli huleta faida
(10-11). Mungu anataka watu wafanyao mambo kadiri ya ujuzi na ukweli.
Hapendezwi na mtu mvivu ambaye siku zote hujitetea tu, au mwanamke asiye na
heshima ambaye hukosesha watu wengine kwa umalaya wake (12-14). Ujinga wa
kitoto unaweza kurekebishwa na nidhamu ya wazazi. Ubahili wa watu wazima
unaowaonea maskini na kuwapa rushwa matajiri kutaadhibiwa (15-16).
0 comments:
Post a Comment